Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Abdurahman Shiloow
Na Mwandishi,
Arusha.
Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Abdurahman Shiloow amelimwagia sifa jiji la Arusha kwa utekelezaji wa miradi mingi na mikubwa ya maendeleo pamoja na ushirikiano mzuri uliopo kati ya ofisi ya Mkurugenzi, Mstahiki Meya pamoja ofisi ya Mkuu wa wilaya.
Mhe. Shiloow ameyasema hayo leo kwenye Mkutano wa Baraza la Madiwani robo ya pili ya mwaka 2022 ambapo madiwani na wataalam kutoka Jiji la Tanga walikuwa kwenye ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo inayotekelezwa na jiji la Arusha.
“Hapa Arusha tuna mengi ya kujifunza, kuanzia miradi mlionayo, uhusiano mzuri kati ya Mkurugenzi, madiwani na Mkuu wa wilaya, lakini kingine ni matumizi ya teknolojia kwa maana ya Kishkwambi, naona kila diwani na wataalamu wa hapa Jiji la Arusha mnatumia Kishkwambi, haya ni mambo muhimu kwetu kuyaiga” Alisema Mhe. Shiloow.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Said Mtanda aliwakaribisha madiwani hao kutoka Tanga na kuwataka kuendelea kutembelea jiji la Arusha ili kujifunza zaidi na kusema siri kubwa ya maendeleo hayo ni uwepo kwa utulivu wa kisiasa miongomi mwao.
Mhe. Mtanda aliwataka madiwani wa Jiji la Arusha kuendeleza utulivu na umoja uliopo ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwani migogoro huchelewesha maendeleo kwa wananchi. Ambapo alisema
“Haya yote yanatokana na utulivu uliopo kwani maendeleo hayataki kelele, kwa hiyo tuendelee kuheshimiana ili kuhakikisha jiji letu linaendelea kuwa mfano wa kuigwa nchini na kubwa zaidi wananchi wetu wapate huduma bora kama serikali ilivyokusudia”
Katika upande wa elimu na mapato, Mkuu wa Wilaya amesema jiji la Arusha linaendelea kuongoza kwani katika matokeo ya darasa la saba kwa shule za serikali, jiji la Arusha limeendelea kuongoza kwa kushika nafasi nne kitaifa mfululizo na katika ukusanyaji mapato awali lilishika nafasi ya kwanza na sasa limeshika nafasi ya pili kitaifa.
Madiwani kutoka jiji la Tanga katika kipindi cha uwepo wao watatembelea miradi mbalimbali iliyopo Jiji la Arusha ikiwemo madarasa ya ghorofa katika shule ya sekondari Arusha Terrat, pamoja na shule ya sekondari Unga Ltd, mradi wa matofali uliopo eneo la Njiro pamoja na miradi ya maeneo ya wazi ya uwekezaji wa vivutio vya utalii Themi Living Garden.
Miradi mingine watakayotembelea ni soko la Machinga kiwanja Na. 68 ulilopo eneo la Kilombero, maduka ya biashara Krokon na Ranger Safari pamoja na eneo la wazi la Levolosi ambapo miradi yote imejengwa kwa fedha za mapato ya ndani za Halmashauri ya Jiji la Arusha.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa