Na Mwandishi Wetu,
Arusha.
Zaidi ya shilingi Milioni mia nne zinatarajiwa kutolewa kwa vikundi vya ujasiriamali 59 kutoka katika Halmashauri ya Jiji la Arusha fedha zinazotokana na asilimia kumi ya mapato yake ya ndani kwenye robo ya pili ya mwaka 2021/2022 kwa lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Jiji la Arusha Dkt. Onesmo Mandike ambapo amewasisitiza washiriki wa mafunzo hayo ambao ni kutoka kundi la wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili watu wengine waweze kukopa.
Dkt. Mandike amesema kuna dhana potofu imejengeka miongoni mwa jamii kuwa mikopo hiyo ni hisani kwamba haitakiwi kujereshwa hivyo kuwataka wanufaika hao kuondokana nayo na kuhakikisha wanarejesha tena kwa wakati ili kila mtu mwenye sifa anayehitaji mkopo huo aweze kupatiwa.
“Lengo la mikopo hii ni kuhakikisha wananchi wote wenye sifa ya kupata mikopo wanapata kwa lengo la kuwainua kiuchumi, ndiyo maana nasisitiza kuirejesha tena kwa wakati kwani hii mikopo siyo hisani kama baadhi ya watu wanavyodhani” Alisisitiza Dkt Mandike.
Amesema jumla vikundi 32 kutoka kundi la wanawake watapatiwa kiasi cha shilingi milioni 164, vikundi 16 kutoka kundi la vijana nao watapatiwa kiasi cha shilingi milioni 164 pamoja na vikundi 11 kutoka kundi la watu wenye ulemavu watapatiwa kiasi cha shilingi milioni 82.
Mratibu Mwezeshaji kutoka Jiji la Arusha Bw. Loishoki Naju amesema mafunzo hayo yanatokana na sera inavyoelekeza kutoa mafunzo kabla ya kutoa mkopo kwa maana ya namna ya kutumia fedha hizo ikiwa ni pamoja na utunzaji wa kumbukumbu, utafutaji wa msoko, ujasiriamali, ufugaJi bora kwa wale wafugaji, pamoja na kuwakumbusha masuala ya UKIMWI.
Mwakilishi kutoka kundi la watu wenye ulemavu ambaye pia ni Katibu wa Shirikisho wa vyama vya watu wenye ulemavu Jiji la Arusha Bi. Eunice Urassa amemshukuru Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kujali makundi yote kwenye masuala mbalimbali ikiwemo fursa za kiuchumi na kuwataka wanufaika wenzake kutomuangusha Mhe Rais kwa kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili waendelee kuaminiwa na kupewa mikopo zaidi.
Halmashauri ya Jiji la Arusha imekuwa kinara wa utoaji wa mikopo inayotokana na asilimia kumi ya mapato yake ya ndani ambapo makundi yote kwa maana ya kundi la wanawake, vijana na watu wenye ulemavu yamekuwa yakipatiwa mikopo hiyo kwa wakati.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa